Na JOHN KIMWERE,
NAIROBI
MALKIA wa handiboli nchini, Nairobi Water Queens sasa wanawazia kampeni za Ligi Kuu muhula mpya.
Kikosi hicho kinazidi kutawala mchezo huo hapa nchini bila kuweka katika kaburi la sahau kipute cha Afrika Mashariki na Kati. Nairobi Water Queens ya kocha, Jack Ochieng wiki iliyopita ilitawazwa mabingwa wa mechi za Super Cup kwa mara ya sita mfululizo.
Kwenye ngarambe hiyo Nairobi Water Queens ilisajili ushindi wa mechi zote tatu dhidi ya Nanyuki Ladies, Jeshi la Ulinzi (KDF) na Nafaka na Mazao nchini (NCPB). Kocha huyo anadokeza kuwa hawana la ziada bali wamepania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha wamehifadhi taji la Ligi Kuu kwa mara ya tisa.
Anasema wachezaji wake kamwe hawana sababu ya kutokaza budi na kuhifadhi ubingwa huo. Ujio wa Nairobi Water Queens ulifunika ufanisi wa NCPB iliyotawala mchezo huo kwa miaka kadhaa.
AFRIKA MASHARIKI NA KATI
Mwishoni mwa mwaka uliyopita Nairobi Water Queens chini ya nahodha, Gladys Chillo iliendeleza ubabe wake iliposhusha ushindani wa kufa mtu na kuhifadhi ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati (ECAHF) kwenye mechi zilizoandaliwa jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Warembo hao walitawazwa malkia wa kipute hicho baada ya kushinda mechi zote nne. Shindano hilo lilijumuisha Nairobi Water na NCPB (Kenya), Ngome na JKT (Tanzania) na Kiziguro ya Rwanda.
”Tunaanza maandalizi ya kushiriki mechi za Ligi Kuu msimu huu baadaye mwezi huu ambapo kamwe hatutawapuuza wapinzani wetu,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa anafahamu wamepania kurejea kivingine.
Anashukuru wachezaji wake na kusema licha ya kupata ushindani mkali nyakati zote wamekuwa ng’ang’ari na kufanya kweli. Pia kocha huyo anasema anataka wachezaji wake wafanye mazoezi ili wawe fiti ili kupata nafasi kuteuliwa katika timu ya taifa itakayoshiriki fainali za kombe la Afrika zitakazofanyika baadaye mwaka huu.
Kocha huyo anasifia wachezaji wake na kutaja kuwa baadhi yao wamekaa vizuri kushiriki handiboli ya kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya. ”Tunatoa wito kwa wahisani wajitokeze na kufadhili ligi ya handiboli nchini kwenye juhudi za kusaidia klabu mahiri Afrika kutambua uwezo wa wachezaji wetu angalau kupata nafasi kujiunga na baadhi yazo,” akasema.
LIGI KUU
Kwenye kampeni za ligi kuu muhula uliopita wasichana hao walishinda mechi zote 14 ambapo waliibuka kifua mbele kwa kuzoa pointi 28, nne mbele ya Ulinzi Sharks. Nao malkia wa zamani, Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) waliridhika na nafasi ya tatu kwa alama 18, moja mbele ya Nanyuki Ladies.
Kocha wa NCPB, Danston Eshikumo anasema ”Wapinzani wetu watarajie kibarua kigumu msimu huu maana tunataka kurejesha uhodari wetu kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.”
Nairobi Water Queens inashirikisha wachezaji kama:Eunice Oginga na Modesta Auma (golikipa). Winga:Glady’s Chilo, Faith Mukhala, Jane Waithera, Cecilia Katheu, na Mercy Katola. Safu ya Kati: Tracy Awino, Rose Ambongo, Mercy , Lucy Auma, Melvin Akinyi, Michele Adhiambo na Brenda Musambai.
SAFU YA NYUMA; Brenda Ariviza, Elizabeth Kemei na Vallarie Adhiambo.
Kamati ya Kiufundi: Jack Habert, Thodosia Sangoro na Caroline Kusa.